Alhamisi 22 Oktoba 2026 - 13:00
Mwanasosholojia wa Ufaransa Achambua Chanzo cha Uporaji Wakati wa Maandamano ya Wananchi

Hawza/ Paolo Stoppa, mwanasosholojia wa Ufaransa, amesema kuwa majina kama “wahuni” na “waharibifu” yanayotumiwa kuwataja baadhi ya waandamanaji ni mbinu zinazotumiwa na serikali kwa ajili ya kuyakandamiza maandamano ya wananchi, ameeleza kuwa chanzo cha uporaji ni pamoja na hasira ya kihistoria dhidi ya alama za ubepari na kushindwa serikali kutatua matatizo ya wananchi, aidha amesisitiza nafasi ya mitandao ya kijamii katika kuimarisha maandamano na kuwawezesha waandamanaji kukabiliana na polisi wa Ufaransa.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Paolo Stoppa, mwanasosholojia wa Ufaransa, amechambua uporaji wa bidhaa na maduka nchini Ufaransa uliofanyika wakati wa maandamano makubwa ya wananchi pembezoni mwa maandamano ya tarehe 17 Oktoba 2026 nchini humo. Amesisitiza kuwa kuwaita watu waliohusika katika matukio hayo “waharibifu” pekee hakuwezi kueleza kikamilifu ukubwa na sura mbalimbali za matukio hayo.

Kwa mujibu wake, kuelewa matukio hayo kunahitaji kuchunguza sababu mbalimbali zinazowasukuma watu kushiriki, historia ya ghasia za mitaani, alama za kiuchumi zilizolengwa, pamoja na nafasi ya mitandao ya kijamii katika kuratibu na kuwawezesha waandamanaji kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa haraka.

Uporaji: Kutoka katika Maandamano ya Kisiasa hadi Fursa za Kujinufaisha Binafsi

Paolo Stoppa, katika mahojiano na chombo cha habari cha Ufaransa cha The Conversation kuhusu uporaji na uharibifu wa mali uliofanyika pembezoni mwa maandamano ya tarehe 17 Oktoba, amesema kuwa jambo linaloweza kuwa halijawahi kushuhudiwa kwa kiwango hicho katika matukio haya ni ukubwa wa uharibifu wa mali binafsi na wizi wa bidhaa.

Hata hivyo, ameeleza kuwa si watu wote walioshiriki katika vitendo hivyo waliokuwa wanahusishwa na makundi yaliyopangwa au mikondo maalumu ya kisiasa.

Mwanasosholojia huyo, akirejelea tafiti zilizofanywa hapo awali kuhusu ghasia za kisiasa nchini Ufaransa, amefafanua kuwa uchaguzi wa maeneo au vitu vinavyolengwa katika vitendo vya ghasia unaweza kuathiriwa na mambo mawili: vikwazo vya kiutendaji na kiufundi, pamoja na utamaduni wa mapambano wa watu wanaoshiriki.

Ili kufafanua suala hilo, amerejelea uzoefu wa miaka ya 1970 nchini Italia na Ufaransa, wakati baadhi ya wanaharakati wa kisiasa walipotumia dhana kama “kupunguza matumizi kwa hiari” na “kuchukua tena mali kwa niaba ya wafanyakazi” ili kuhalalisha kuchukua bidhaa na huduma muhimu.

Kwa mujibu wa Stoppa, mojawapo ya mifano maarufu ya vitendo hivyo ni wizi uliofanyika mwezi Mei 1970 katika duka la vyakula vya kifahari la Fauchon, lililoko katika uwanja wa Madeleine jijini Paris. Katika tukio hilo, bidhaa zilizosombwa ziligawiwa kwa wakazi wa makazi duni na maeneo ya makazi ya wafanyakazi.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa haiwezekani kusema kwamba uporaji wote uliofanyika tarehe 17 Oktoba ulikuwa na malengo ya kisiasa. Kusambazwa video za vitendo hivyo kwenye mitandao ya kijamii na kuuzwa tena baadhi ya bidhaa zilizoibwa kupitia tovuti za intaneti ni miongoni mwa ushahidi unaofanya iwe vigumu kutoa tathmini moja kuhusu sababu zilizowasukuma wahusika wote.

Alama za Ubepari na Malengo Tofauti ya Uporaji

Stoppa, akizungumzia ukweli kwamba baadhi ya maeneo yaliyolengwa wakati wa matukio ya tarehe 17 Oktoba yanaonekana kutolengwa kwa bahati mbaya, amesema kuwa baadhi ya taasisi zilizoshambuliwa ni alama za ubepari. Taasisi hizo ni pamoja na maduka ya bidhaa za kifahari, kampuni za bima, benki na mashirika ya kimataifa.

Mbali na taasisi hizo, baadhi ya maduka madogo ya mitaani na ya wenyeji, yakiwemo maduka ya vifaa vya kuchezea watoto na maduka ya michezo ya video, nayo yalilengwa. Kwa mujibu wa mwanasosholojia huyo, maeneo ya aina hii si mara nyingi huwa miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na vitendo kama hivyo.

Ameongeza kuwa; tangu kuibuka harakati za kupinga utandawazi, katika baadhi ya matukio, ghasia dhidi ya mali zimeelekezwa dhidi ya alama za ubepari, hususan mashirika ya kimataifa.

Hata hivyo, amesema kuwa vitendo vya aina hiyo pia hujitokeza sambamba na vitendo vya ghafla vinavyofanywa na makundi ya watu wasio na mwelekeo maalumu wa kisiasa, ambao hujitokeza pembezoni mwa maandamano kwa lengo la kujipatia bidhaa kwa kuzichukua kutoka katika maduka.

Historia ya Kutumiwa kwa Jina la “Waharibifu” Katika Maandamano ya Wananchi Nchini Ufaransa

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, mwanasosholojia huyo amezungumzia historia ya matumizi ya istilahi “waharibifu” katika uchambuzi wa maandamano nchini Ufaransa. Amesema kuwa mwanasosholojia Guénola Ricordeau alikuwa miongoni mwa watafiti wa kwanza kuchunguza jambo hilo.

Kwa mujibu wake, katika miaka ya 1990, kwa mfano wakati wa harakati za wanafunzi wa shule na vyuo mwaka 1998, ilibainika kuwa baadhi ya vijana walishiriki katika mikusanyiko bila kuunga mkono madai ya waandamanaji. Badala yake, walihudhuria mikusanyiko hiyo ili kuharibu mali au kuwaibia watu.

Stoppa amefafanua kuwa ushiriki wa watu hao ungeweza kusababishwa na kutaka kutumia fursa zilizojitokeza kwa manufaa yao binafsi au hamu ya kujinasua katika maisha ya kila siku yenye mazoea yaleyale. Jambo hilo linaonesha kuwa vitendo vya ghasia vinavyotokea pembezoni mwa maandamano si lazima viwe vinatokana na sababu moja inayofanana au mwelekeo mmoja wa kisiasa.

Aidha, amehusisha hali hiyo na machafuko yaliyotokea katika vitongoji vya pembezoni mwa miji na maeneo yenye hali duni ya kiuchumi nchini Ufaransa, ambayo yalianza kuenea hatua kwa hatua kuanzia nusu ya pili ya miaka ya 1970.

Kwa mujibu wake, istilahi “waharibifu” ilipata mwangwi mkubwa katika vyombo vya habari wakati wa machafuko ya mwaka 2005 nchini Ufaransa. Jina hilo lilitumiwa kuelezea vijana waliokuwa wakishambulia vikosi vya polisi, mali binafsi na miundombinu ya umma, ikiwemo vifaa vya mijini. Hata hivyo, katika mtazamo huo, uwezekano wa vitendo vyao kuwa na maana au malengo ya kisiasa haukupewa uzito wa kutosha.

Mitandao ya Kijamii na Ugumu wa Kudhibiti Harakati za Waandamanaji

Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Stoppa amesisitiza nafasi ya mitandao ya kijamii katika mabadiliko ya hivi karibuni, akisema kuwa namna ya kutumia mitandao hiyo imebadilika ikilinganishwa na miaka ya 2000.

Kwa mujibu wake, hapo awali mitandao kama Facebook, Instagram na Twitter ilitumika pamoja na baadhi ya zana za kutuma ujumbe. Hata hivyo, siku hizi zana kama Snapchat na Telegram pia zimewezesha mawasiliano ambayo, katika baadhi ya mazingira, ni vigumu zaidi kuyafuatilia na kuyachunguza kutokana na muda mfupi ambao ujumbe hubaki au vikwazo vya upatikanaji wake.

Akizungumzia kuundwa kwa makundi ya mazungumzo ya wazi na ya faragha, pamoja na mitandao midogo ya mawasiliano yenye wanachama wachache, amefafanua kuwa mitandao hiyo inaweza kuwezesha kubadilishana taarifa kwa haraka na kutoa msaada wa papo hapo kwa waandamanaji walioko katika maeneo ya maandamano.

Stoppa ameongeza kuwa katika mazingira hayo, watu wanaweza kuhama kwa haraka kutoka sehemu moja kwenda nyingine na, kupitia mawasiliano yenye usiri wa kiasi, kujikusanya katika maeneo mbalimbali na kusaidiana. Hali hiyo inaweza kuifanya iwe vigumu kwa vikosi vya polisi wa Ufaransa kuwatambua na kuwakamata au kuwazuia.

Kwa mujibu wa mwanasosholojia huyo, sifa za kiufundi za baadhi ya mitandao ya kijamii na mifumo inayohusiana na akaunti za watumiaji zinazotumiwa na waandamanaji zinaongeza ugumu wa hali hiyo. Amesisitiza kuwa muunganiko wa kasi ya kubadilishana taarifa kwenye mitandao ya kijamii na uwezo wa waandamanaji kuhama kwa haraka unafanya udhibiti wa makundi hayo kuwa mgumu zaidi.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha